Halloween Costume ideas 2015

KAZI YA SHETANI -2

JINA LA HADITHI – KAZI YA SHETANI
SEHEMU YA         - PILI
MWANDISHI        - ASLAM KHAN
aslamstorymail@gmail.com
aslamstori.blogspot.com

Iliposhia…

Sikujua ni muda gani ulipita mpaka pale usingizi uliponipitia na kulala kabisa. Ila nilikuja kuamka majira ya kama saa nane ama tisa hivi za usiku, hiyo ni kutokana na makadirio yangu tu. Nilistuka sana pale nilipofungua macho. Nilikuwa katika sehemu ambayo sikuifahamu kabisa

Endelea…

Sehemu ngeni machoni kwangu. Sehemu ambayo mazingira yake sikuwahi kuyaona kabla wala kuyasikia yakisimuliwa. Yalikuwa ni mazingira ya ajabu mno kwangu. Yalionekana mazingira yenye rangi nyeupe. Ardhi yake ilikuwa nyeupe kabisa kana kwamba ilikuwa imezingilwa na theruji, badala yake haikuwa theruji
kwa sababu hakukuwa na hali ya maji maji katika ardhi hii wala kiasi cha baridi chenye kufanya ardhi itandwe na theruji, nilistaajabu sana.
Niliangaza huku na huko bila kufanikiwa kuiona nyumba wala watu. Nilikuwa nipo katika sehemu ya jangwa jeupe. Jangwa lisilo na mchanga wala jua kali. Taratibu nilijiinua tokea pale chini na kuanza kutembea kwenda sehemu ambayo sikuwa ninaifahamu. Sikufahamu wapi nilipokuwa ninaelekea kama ndo ulikuwa upande sahihi wala sikufahamu ule ulikuwa ni upande gani wa dira. Sikuliona jua wala mwezi hivyo kushindwa kukadiria kuwa huo ulikuwa ni wakati gani. Kulionekana kuwepo kwa mwanga uliotosha kuyaona mazingira ama watu vizuri lakini hata nilipoangalia juu, sikuweza kuona chanzo cha mwanga huo. Hakuna mbingu ya bluu kama nilivyozoea. Nilitembea taratibu huku nikiendelea kuangalia huku na huko kuona kama naweza kuona hata mtu ambaye angeweza kuyajibu maswali yaliyokuwa yametawala ubongo wangu na ikiwezekana aweze kunipatia msaada, sikuweza kuona mtu.
 Niliendelea kutembea pasi na kujua nini hatma yangu, huku nikiangaza huku na huko bila ya kuona chochote. Baada  ya kutembea  kwa takribani dakika  kama arobaini hivi bila kujua kule nielekeako, ndipo sasa nuru ilipoanza kunijia usoni kwangu. Sio nuru ya mwanga, la hasha! Ni nuru kwa sababu nilianza kukutana na watu wakiranda randa huku na huko. Walikuwa watu wa ajabu sana. Sikuweza kuziona nyuso zao kwa sababu nilikuwa zimetawaliwa na nuru ya ajabu , hazikuweza kutambulika kiurahisi. Nilijikuta nipo katika kiza chenye mwanga. Mwili na mavazi yao yote yalikuwa meupe kabisa kama ambavyo yalivyokuwa mazingira yao. Nilistaajabu na taratibu woga ukaanza kunijia. Nilipiga moyo konde na kujaribu kuwasemesha, lakini hakuna hata mmoja aliyepata kusimama japo kunisikiliza tu achilia mbali kunijibu kwa kunisemesha. Nilizidi kuogopa sana. Nilijikaza kiume na kuendelea na safari yangu huku nikifuata kule ambako kulionekana kuwepo kwa wale viumbe kwa wingi. Nawaita viumbe kwa sababu sifahamu kama ni watu au la! Nilianza kuziona sehemu za makazi ya viumbe hao, lakini ajabu ni kuwa hadi nyumba nazo zilikuwa zikionekana kuwa na rangi ile ile, nyeupe. Hali ile ilinichanganya sana. Ilikuwa hali ngeni nay a kustaajabisha mno. Niliendelea kutembea kwa takribani kilomita moja hivibila ya kupata msaada wa aina yeyote ile. Nikiwa katika hali ya kukata tamaa huku nikiangaza huku na kule, ghafla nilipata tumaini, tumaini jipya, taratibu hofu yangu ilianza kupungua, furaha ikaanza kunijia. Hiyo ni kwa kile nilichokuwa nimekiona, sikuamini macho yangu, nilifikiri labda nilikuwa ninaota, lakini ilikuwa ni kweli, wala haikuwa ndoto.
                                 
                                      ***********************************
Kulionekana kuwepo kwa kikao   au mkutano wa siri miongoni mwa wananchi wa Kopsheng. Wengi wa wananchi hao walionekana walikuwa ni wapingaji wakubwa wa utawala uliokuwa ukitawala katika eneo hilo. Yule aliyeonekana kuwa ni kiongozi wa waasi hao kama ambavyo hujulikana alisimama na kufungua mkutano wakiwa katika sehemu yao ya maficho.
“wapendwa, kwa mara nyengine tena tumekutana hapa kama ilivyo desturi yetu ili kujadiliana juu ya lile suala letu la siku zote lenye kutufanya tukutane hapa….” Alisema akakohoa kidogo na kuendelea
“….wote nafikiri munatambua ni kitu gani kilichotuleta hapa, kwa hiyo siwezi kurudia tena kuelezea ili tujadiliane mambo muhimu, si mutajua muda ni mdogo sana?” Yule kiongozi alisema akiachia swali kwa washirika wa ule mkutano wa siri. Wengi wao walionekana kuitikia kwa kuchezesha kichwa kuonyesha kukubaliana na maneno ya kiongozi wao.
“…..Leo kuna kitu kipya……” alisema  na kuendelea
“….kuna tatizo, tatizo kubwa  sana, kwa uwezo mdogo wa kufikiri inawezekana likaonekana ni tatizo dogo, lakini matokeo mabaya yanaweza kuja kutokea hapo baadae, kwa hiyo nimewaita hapa ili tujadiliane kujua ni kwa namna gani tutaweza kulitatua ingawa nahisi itachukua muda sana!” Alimaliza huku akiwaangalia  washirika wa ule mkutano akiashiria kutaka kusikia neno kutoka kwao.
“Ni tatizo gani tena kiongozi?” aliuliza mmoja wa washiriki wa ule mkutano.
“Je kuna hata mmoja kati yenu ambaye anajua ni kitu gani hasa nilikuwa nimekipanga kukifanya ili kuwasaidia wananchi wetu?” aliuliza.
Ilionekana washirika wa ule mkutano walikuwa wameulizwa swali gumu mno kiasi ya kwamba badala ya kutoa majibu yake, bali ikaanza kusikika ninong’ono  kati yao.
“mmmhgh mmmhg…!” kiongozi alijikohoza baada ya kupita takribani sekunde arobaini na tano za minong’ono. Wote wakanyamaza kimya ili kumsikiliza kiongozi wao.
“…mimi nimeuliza ili nijibiwe, sasa mkianza kunong’ona bila kutoa majibu, tutajikuta muda umetuishia na hakuna cha maana ambacho tutakachokuwa tumekijadili, na badala yake kuonekana mkutano wetu huu hauna faida!” alisema akiendelea kuwaangalia akisubiria jibu.
“hapana..hapana…hapana!” walijibu huku wakisisitiza kuwa hakuna kitu ambacho walikuwa wakikifahamu.
“Tush…!” Yule kiongozi aliita jina la mmoja wa washiriki waliokuwemo ndani  ya eneo la mkutano na alionekana akiinuka na kusimama.
“ndio kiongozi!”
“kwanza  ongera sana kwa kutunza siri hii niliyokwambia juzi na hakuna hata mmoja aneyejua kile nilichokuwa nimekipanga. Naweza kusema kuwa huu ulikuwa ni mtihani mkubwa kwako na naweza kusema kuwa umeufaulu kwa asilimia zote, ongera sana!” 
“ahsante sana kiongozi!”
“ila pia nimestaajabu sana kuona kuwa hata wewe ni umekuwa ni miongoni mwa watu wasiojua kile nilichokipanga!”
“samahani sana mzee!” Tush aliomba msamaha
“huo ndio uamini  wenyewe tunaouhitaji ili kuweza kuichukua nchi hii na kuiweka katika sehemu sahihi zaidi ya hapa tulipo kwa sasa hivi. Uaminifu unauweka mbali usaliti, ooh kwa hiyo hakuna kosa ulilolifanya lenye kukuwajibikia kuomba msamaha Tush, ila nakusifu kwa kile ulichokifanya. Ongera sana!”  alisema na kukohoa kidogo na kuendelea
“Wananchi  wa Kopsheng, mlioamua kuwasimamia wanachi wengi wa nchi yetu hii ambao hawajui nini hatma yao itakavyokuwa kesho, napenda kuwashukuru sana kwa ushirikiano wenu wa karibu  na kufika kwenu kila pale munapokuwa munahitajika. Tunahitajika tushikamane pamoja ili kufanikisha lile tuliloamua kulianzisha kuhusu kinachoendelea nchini kwetu. Sasa kwa kifupi ni kuwa nilikuwa nimepanga kuwaleta viumbe ambao wana uwezo mkubwa sana wa kufikiri na kutendamambo kwa kutumia akili zaidi kuliko kutenda bila ya kujua matokeo ya matendo yao.” Alisema kiongozi wa waasi.
“Kwa akili zaidi kuliko sisi?” aliuliza mmoja wa washiriki wa mkutano ule wa siri.
“sio kwamba siku zote dawa ya moto ni moto tu, hapana dawa ya moto kwa tafsiri rahisi ni maji, moto ukiwaka chukua maji na uuzime, viumbe hao ni tofauti na sisi, hivyo itakuwa ni rahisi sana kwetu kupata msaada kutoka kwao. Viumbe hao wanao uwezo wa kutafuta mbinu sahihi ya kukitawala kiumbe chochote na kwao hakuna kiumbe kinachowasumbua hasa kama watawezeshwa kwa ufundi Fulani Fulani hivi.” Alisema
“kiongozi wetu, sisi huwa hatukupingi mara nyingi kwani maamuzi ambayo huwa unayachukua huwa na matokeo mazuri baadae, ila swali langu ni kiumbe gani huyo ambaye umefikiria kumleta ili kutusaidia katika suala letu la kuirudisha nchi kule ilikotoka kwenye asili yetu watu wa Kopsheng?” mshirika mwengine aliuliza.
”Binadam, binadam ndio viumbe ambao nimefikiria kuwaleta ili kutusaidia kukabiliana na matatizo yanayotukabili” kiongozi alibainisha.
“binadam?!.....” aliuliza mmoja wao kwa mshangao akaendelea.
Je kwa nini ameuliza kwa mshangao kama hivyo na hao watakuwa ni sahihi au sio?
Fuatilia sehemu inatofuata

Labels:

Post a Comment

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget