Halloween Costume ideas 2015

KAZI YA SHETANI -10


JINA LA HADITHI – KAZI YA SHETANI
SEHEMU YA         -KUMI
MWANDISHI        - ASLAM KHAN
aslamstorymail@gmail.com
aslamstori.blogspot.com

Iliposhia…

“hebu tuondoke hapa, twende tukakae na wenzetu wanaweza wakatufikiria vibaya!”
“kutufikiria vibaya, kwani kuna mtoto mdogo hapa kati yangu na wewe?”
“hakuna, ila haipendezi, kuwaacha peke yao harafu sisi tunajitenga huku, kama yule mzee akirudi asije kupata tabu tena ya kuanza kututafuta, kwanza alisema tusitoke pale!”
“sawa, wewe ndiye umeshinda, twende!” nilimuambia toka pale katika jiwe na taratibu tukaanza kurejea kule ambako mzee alituacha na kutuambia tusitoke.
“Aziza!”
“ndio!”
“hivi jina lako la kweli ni nani?” nilimuuliza

Endelea…

 “Aziza Abeid Swalehe!”
“wewe ni muislamu kumbe?”
“swadakta (umesema kweli) kabisa!”
“vizuri sana, wewe ni mtoto wa ngapi katika familia yenu?”
“mimi ni mtoto pekee katika familia yetu, baba yangu inasemekana alifariki wakati nilipokuwa na umri mdogo sana!”
“pole sana, je alikuwa anaumwa?”
“hapana, ni ajali tu!”
“ajali ya gari au?”
“hapana, baba yangu alikuwa anaenda kuwatetea wananchi nje ya dunia yetu sehemu moja inayoitwa Kopsheng. Akiwa na wenzake, walizidiwa nguvu na kiongozi wa waasi na badala yake ufalme ukachukuliwa na yule kiongozi wa waasi!”
“aaah, kwa hiyo hata huyo mfalme atakuwa ameuawa?”
“sina taarifa sahihijuu ya hilo, mara nasikia ni mzima mara nasikia ameuliwa, sina uhakika kabisa!”
“dah, pole sana!
“ahsante sana, niliapa lazima nikalipize kisasi cha baba yangu hivyo mama alinipatia mafunzo ya kutumia upanga katika mapambano na kuniambia pindi nitakapofikisha umri wa miaka kumi na nane ndio utakuwa ni umri sahihiwa kulipiza kisasi changu!” 
“sasa una umri wa miaka kumi na nane, utalipizaje kisasi sasa?”
“ndio maana nakuwa mpole sana huku ili niweze kurudi duniani mapema mno nipate kumuuliza mama yangu ni kwa jinsi gani nitakavyoweza kulipiza kisasi na kupata miongozo yote kutoka kwake!”
“kwa hiyo una uwezo wa kupambana kwa kutumia mapanga, si ndivyo?”
“ni kweli, sio hivyo tu bali pia nilifundishwa elimu ya gizani ambayo naweza kuitumia kwa kujillinda na adui!”
“Ina maana unatumia na unaujua uchawi wewe?”
“ndio, je unataka nikufundishe?”
“hapana, hapana, hapana, labda unifundishe kupambana kwa kutumia mapanga tu!”
“njoo ujaribu, ni dakika ishirini tu utajiona jinsi utakavyokuwa, hebu tafuta fimbo ndefu mbili zenye urefu wa mkuki!”
Nilianza kutafuta hizo fimbo kwa takribani dakika tano bila ya mafanikio.
“sijazipata!”
“tumia akili ya kuzaliwa nayo wewe!”
“niambie”
“hii itakuwa ni mara ya kwanza na ya mwisho kukumbusha, umenielewa?”
“sawa!”
“tumia hiko kisu sasa!”
“nakitumiaje sasa?, sijui!” nilimuuliza huku nikiwa nimekishika kisu mkononi.
“acha upuuzi, tumia hisia zako!”
“.......inafanya kazi kutokana na fikra za mtu. Ina uwezo wa kugeuka kila aina ya silaha endapo nafsi yako ikikubalika na nafsi ya hiyo fimbo!” niliyakumbuka maneno ya yule mzee.
Nilikishika kile kisu vizuri na kuweka hisia zangu na kukiamuru kigeuke na kuwa fimbo. Kutahamaki, fimbo nyingi zilitokea na kudondoka chini huku mkononi nikiwa nimebakiwa na fimbo moja.
“upuuzi huu, hhahahahaha!” alisikika Aziza akisema huku akinicheka.
Alikuja na kuninyang’anya ile fimbo niliyobakiwa nayo mkononi na kutahamaki fimbo zote zilipotea na kubakia fimbo moja pale chini. Alinipatia ile fimbo aliyoichukua toka mikononi mwangu na kisha yeye akaokota ile fimbo iliyokuwa ipo ardhini.
“kumbe na wewe una uwezo wa kukitumia hiki kisu?” nilimuuliza kwa mshangao.
“ndio!”
“kwani wewe ni nani?”
“utanitambua baadae, ila si unajua kama mimi ni Aziza?”
“hapana sio hivyo, nahisi kama kuna kitu unachokijua zaidi!”
“wewe ndiye uliyesema, sio maneno yangu hayo. Hakuna kitu chochote ninachokijua zaidi ya kuwa nimepotea huku na inanipasa kurudi nyumbani haraka iwezekanavyo ili niweze kulipiza kisasi kwa wakati muafaka!”
“siamini!”
“hebu shika vizuri hiyo fimbo!” alisema Aziza
Niliishika fimbo yangu vizuri tayari kwa mafunzo.
“kwa sababu wewe pia una nguvu za miujiza tayari, basi haitokuwa kazi ngumu sana!” Aziza aliniambia.
“nguvu za miujiza?, ninazo mimi au?” nilimuuliza kwa mshangao.
“ndio, unazo, ila tatizo ni kuwa hautambui hilo na wala haujui jinsi ya kuzitumia, ila nitakuonyesha!” alisisitiza Aziza.
“duh...!”
“shika fimbo yako hivi...!” alisema Aziza akinionyesha jinsi ya kuishika fimbo vizuri.
“utafuata kwa vitendo kile nitakachokuwa ninakifanya, sawa?”
“sawa!”
“tunaanza, weka mwili wako kama nilivyosimama mimi!”
“sawa.....!”
“kushoto.....kulia.....kati.......kushoto.....”. alisema Aziza huku akiipeleka fimbo yake kulia, kisha kushoto, kisha aliruka kidogo na kuwa kama mtu anayepasua kuni katikati kwa kutumia shoka. Nami nilimfuatisha kwa vile alivyokuwa anafanya.
“......mbele.....nyuma....ngao....ulinzi.....” aliendelea kusema huku ukiinyoosha fimbo yake mbele, kisha akarudisha mikono nyuma kisha akaisimamisha fimbo yake kimshazari na mwili wake. Kila hatua aliyokuwa anaifanya, niliifuatisha kutokana na maelekezo yake. Tuliendelea na yale mazoezi kwa takribani robo saa hivi. Nilitegemea ingekuwa ni mazoezi magumu mno kwangu hasa kutokana na tabia yangu ya kutopendelea kufanya mazoezi mara kwa mara. Lakini mambo yalikuwa ni tofauti kabisa. Nilijiona nilikuwa mwepesi kwa kila ambacho nilikuwa nafikiria kukifanya, tena nilifanya kwa usahihi wa asilimia mia. Kwa kweli nilistaajabu sana!
“vipi Aziza!” ilikuwa ni sauti ya Hamza iliyotustua na kutufanya tukatishe kile tulichokuwa tunakifanya.
“safi tu, karibu!”
“ahsante, naona unampatia mafunzo!”
“yeah, natimiza wajibu wangu!”
“ni vizuri, kwa sababu matatizo yanakuja kuanza muda si mrefu!”
“matatizo?!” niliwauliza kwa mshangao.
“hamna bwana, anatania tu!” alisema Aziza
“hapana, nyinyi kuna kitu munachokifahamu, siwaelewi kabisa yaani!” nilisema kwa kuhamaki.
“huyu mtoto mbishi sana!” alisema Aziza
“muache bwana, atakuja kuelewa baadae, wewe endelea kumfundisha!” alisema Hamza.
“sitaki kufundishwa!”
“kwa nini hautaki?” aliuliza Aziza.
“sina haja ya kujua zaidi, kinatosha kile ulichonipatia!” nilisema
“hapana, bado kabisa!”
“mimi sitaki sasa!” 
“kweli?”
“ndio!”
“mimi nataka tumalizie kama dakika kumi tu!”
“sitaki, inatosha!”
“sogea!” alisema Aziza nami bila ya kubisha nilimsogelea kwa kujiamini. Alinishika kichwa kwa mikono yake miwili na kufanya umbali kati yangu na yeye kupungua. Alisogeza kichwa chake karibu yangu na kuipeleka midomo yake karibu na sikio langu.
“sikia, kama haukijui kile ninachokijua mimi, sahau kupata penzi toka kwangu. Sahau kabisa ndoto za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mimi. Tena iwe ni ndoto ya mchana ambayo mara nyingi haiwi ya kweli wala haitokei.kikubwa tambua kuwa kauli ya mwisho ndio inayochukuliwa kama ndio amri ya maamuzi jeshini!” alininong’oneza.
                                                                            ***************************


Itaendelea
Labels:

Post a Comment

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget