Jina la Hadithi - Kazi ya Shetani
Sehemu ya - Kwanza
Mwandishi - Aslam Khan
Mawasiliano - +255 (0) 627 676 104
aslamstorymail@gmail.com
aslamstori.blogspot.com
Ilikuwa siku ya jumapili moja iliyo tulivu hasa ukizingatia kuwa ilikuwa siku ya mwisho wa juma. Watu walionekana sehemu mbali mbali wakiwa wawili wawili kana kwamba walikuwa wamezaliwa mapacha. Walifurika sehemu mbalimbali za starehe. Watoto nao hawakubakia nyuma nao walionekana wakiranda huku na huko wakiwa na furaha huku wengi wao wakiwa na mapulizo. Lakini hali ilikuwa ni tofauti kwa upande wangu kwani siku hiyo nilikuwa nasumbuliwa na homa. Nikiwa peke yangu nyumbani, niliendelea kuwaangalia wapita njia walioonekana kuwa na furaha mno. Hapa nilipokuwa ninaishi, nilikuwa ninaishi mimi pamoja familia ya mjomba akiwepo mkewe na mtoto wao mdogo mwenye umri wa miaka mitano. Ilipofika majira ya saa kumi alasiri hali ya hewa ilianza kubadilika kwangu, nilianza kuhisi baridi hali iliyonifanya nianze kutetemeka. Nilijitahidi kujikaza ili niyafaidishe macho yangu kutokana na mazingira mazuri ya siku hiyo yaliyopambwa na watu mbalimbali kutokana na rangi zao za nguo. Nilijitahidi kuvumilia lakini nilishindwa hivyo ikanibidi kuingia ndani na moja kwa moja nikaingia chumbani kwangu ili kujipumzisha. Nilifika chumbani kwangu na kujitupia tu kitandani. Taratibu usingizi wa uchovu na homa ulianza kuninyemelea. Ilipofika takribani saa kumi na mbili kasoro robo, kwa mbali niliwasikia mjomba akiwa na shangazi wakiwa wamerejea kutoka kazini. Baada ya hapo nilipitiwa na usingizi kabisa.
“abdamm.........abdam!” ilikuwa ni sauti ya shangazi akiwa anagonga mlango wa chumba changu.
Wakati huo ilikuwa yapata majira ya saa moja ya usiku.
“abdam....abdam.....abdam!” shangazi aliendelea kugonga mlango huku akiwa ananiita. Kutokana na uchovu uliotokana na homa niliyokuwa nayo, nilishindwa kumjibu shangazi.
“abdam...abdam!” shangazi aliendelea kuita mara baada ya kuona sijibu kitu.
“naaaa....aaaam!” niliitikia kwa uchovu uliopitiliza.
“njoo ule chakula ili umeze dawa!” shangazi alisema kwa msisitizo.
“mmmmh, haiwezekani chakula kiwe tayari saa moja hii!” niliwaza ila niliamua kumjibu
“naa...anaku...ja” nilijibu kiuvivu.
Zilipita takribani dakika ishirini hivi bila ya mimi kutoka chumbani kwangu wala kitandani. Nilikuwa ninajihisi ni mtu mwenye uchovu mno.
“ngoo...ngo...ngoo” ilikuwa ni baada ya kupita dakika takribani ishirini sauti ya mlango kugongwa tena ilisikika.
“mmmmmh...mmmmmhhhgg......mmmhhh” nilijigeuza geuza tu pale kitandani niliposikia mlango ukiwa unagongwa.
“abdam!” shangazi alikuja kuita tena.
“mmmmmh....” nilliitikia kwa uchovu.
“amka uje ule chakula!” alisema.
“naa kuja!”
“uje sasa hivi ule chakula cha moto kabla hakijapoa”
“sawa nakuja!” nilijibu huku nikijaribu kuinuka lakini mwili ulikuwa umechoka mno hivyo nikaamua kujipumzisha kidogo ndipo niende nje. Nikapitiwa na usingizi.
******************************************************
“chakula kimechelewa sana leo, mpaka mtoto anataka kulala chakula bado” alisema mjomba mara baada ya kumuona mtoto wake wa kike aitwae Hajra akiwa anasinzia.
“kimechelewa wakati chakula kipo tayari hapa!” shangazi alijibu
“kimeivaje Wakati bado kipo jikoni hata kupakuliwa bado?”
“hiki tayari bado kidogo tu”
“ mbona haueleweki, mara tayari mara bado nilielewe lipi sasa, angalia mtoto anataka kulala huyu na sijui kama hata kuoga kama ameoga!”
“kwani wote si tumerejea pamoja hapa nyumbani?, wewe muogeshe tu binti yako!”
“oooooh hizo sasa ni dharau nitaanzaje mimi kumuogesha mtoto?”
“kwa nini?”
“mimi ni mwanaume bwana, kumuogesha mtoto na mimi ni wapi na wapi?” aliuliza mjomba kwa mshangao.
“nani aliyesema kama mwanaume hawezi kumuogesha mtoto?”
“mimi ni mwanaume na siwezi kufanya kazi za kike, umenielewa?”
“kumuogesha binti yako ndo kazi ya kike?”
“Hiyo ni kazi yako”
“hivi wewe mwanaume kumuogesha binti yako ni kazi ya kike, je utaweza kumfulia nguo kweli?”
“hahahahaha hebu usiniletee utani wa kunifurahisha hapa!”
“hivi huwa haumuoni baba John vile anavyofanya kwa familia yake?”
“anafanyaje?”
“huwa anafua nguo za mkewe, za mwanawe na Wakati mwengine hata kupika pia. Yote ni kumsaidia mkewe, ila mimi hata sina bahati hiyo.”
“hivi nani asiyejua kuwa huyo baba John amewekwa hapa!” alisema mjomba huku akionyesha katikati ya kiganja cha mkono.
“hizo ni imani zenu tu, na ni imani za potofu”
“zipi imani potofu!”
“hizo unazoziamini wewe, hata sijui kwa nini watu huwa munapenda kuwa na imani za kishirikina, yaani mtu kuamua kumsaidia mkewe ili kuijenga familia iliyo bora basi eti karogwa, wangapi sasa watakaokuwa wamerogwa?”
“hata wakiwa wote!”
“kitabu gani ambacho kiliandika kuwa kufua au kumuogesha mtoto ni kazi za mwanamke?”
“hebu usiniulize hayo maswali yako, fanya haraka umalize kupika nile nikalale!”
“basi naomba tufanye jambo moja!”
“jambo gani?”
“njoo umalizie kupika ili nimuogeshe mtoto!”
“hizo sasa ni dharau zilizopitiliza, ni dharau za reli kiwango cha standard gauge!”
“mimi sikudharau, ila wewe unaona hivyo, najaribu kurahisisha kazi, njoo upike bwana mume wangu nimuogeshe mtoto basi!” shangazi alisema huku akimuangalia mjomba kimahaba na kufanya macho yake makubwa yaliyo meupe kuongeza urembo wake.
“aaaah huko sasa ni mbali sana, hebu niandalie tu hayo maji nimuogeshe”alisema mjomba kwa unyonge. Shangazi aliandaa maji kwa ajili ya kumuogeshea mtoto na kisha akampatia mjomba tayari kwa kumuogesha mtoto.
“na hiko chakula ufanye haraka tumpatie mtoto ale, akalale!” alisema mjomba.
“sawa mume wangu!”
“harafu vipi kuhusu abdam?”aliuliza mjomba
“amelala, anajisikia vibaya”
“aha, sawa kamuamshe kabisa ili aje kusubiria chakula”
“sawa mume wangu ila nilishaenda kumuita kabla, ngoja niende tena!” alisema shangazi na kuinuka kuja karibu na mlango wa chumba changu kwa ajili ya kuniamsha. Aliita bila ya mafanikio, akaamua kwenda kuandaa chakula kwanza.
*************************************************
“ngooo.....ngooooo.....ngoooo” ulikuwa ni mlango uliotii kwa kutoa sauti mara baada ya kugongwa.
“abdam, chakula tayari njoo ule upate kumeza dawa!” shangazi alikuja kuniita tena. Kimya.
“ngooo...ngooo..ngongongo.... abdam....!” shangazi aliendelea kugonga huku akiendelea kuita.
“mmmmmmmmmh.....” nilijigeuza pale kitandani kutokana na kero zilizotokana na kelele za mlango uliokuwa unagongwa.
“amka uje ule chakula ili upate kumeza dawa”
“nakuuu....kuuja” niliitikia katika hali iliyokuwa imetawaliwa na uchovu sana.
“fanya haraka, uje ule chakula cha moto”
“sawa!” nilijibu pasi na kutoka nje. Zilipita dakika kadhaa bila ya kutoka nje.
“ngoongongongo!” ilikuwa ni sauti ya mlango wa chumba changu ukiwa unagogwa lakini safari hii uligongwa kwa nguvu mno.
“abdam hebu toka nje bwana!” ilisikika sauti ya mjomba.
“nakuja mjomba”
“hebu jikaze, fanya haraka utoke nje uje ule, wewe mwanaume bwana.” Alisema mjomba huku akiendelea kugonga mlango kwa fujo.
“nakuja!” nilijibu huku nikiinuka toka kitandani. Nilitoka nje ya chumba changu na kumkuta mjomba akiwa mlangoni akinisubiria.
“acha kujilegeza, wewe mtoto wa kiume!”alisema mjomba huku akinishika begani na kunitingisha.
“anaumwa bwana, hebu muache huko, kwa nini hauna huruma kwa binadamu wenzako?” shangazi alitetea.
“endelea kumtetea tu, mwanaume huyu, kuna vita, ataweza kupigana huyu?” aliuliza mjomba.
“nina imani ataweza zaidi ya kupambana!” shangazi alijibu na kumfanya mjomba apandwe na hasira. Aliamua kwenda mezani na kuanza kula.
Taratibu na mimi nilielekea sebuleni ili kupata chakula cha usiku.
“kula umeze dawa”alisema shangazi kwa sauti ya upole iliyojaa huruma.
“acha kumdekeza bwana!” mjomba alidakia.
“haujaacha tu, hebu kuwa na huruma huko”shangazi alitetea.
“endeleeni” alijibu mjomba na kunawa mikono yake.
“kulikoni tena na wewe?”
“nimeshiba”
“umekula wapi, mbona chakula kipo vile vile tu, au tayari umeshakula kwa watu wako huko”
“umeshaanza hivyo!”mjomba alijibu na kuingia chumbani kwake.shangazi hakuwa na neno jengine la kuongezea.
“muache bwana, we kula hapo umeze dawa.” Alisema shangazi huku akizungusha macho yake makubwa na kumfanya aonekane mrembo mno hasa kutokana na mwanga hafifu wa mshumaa.
“sawa shangazi”
Shangazi alikuwa nakula kwa mapozi hali iliyonifanya ubongo wangu upagawe kutokana na mvuto wake aliokuwa nao. Nilikula chakula na nilipomaliza shangazi alinipatia dawa za maumivu na kuzimeza. Nilipomaliza niliingia chumbani kwangu kwa ajili ya kujipumzisha usiku huo.
***********************************************************************************************************
Sikujua ni muda gani ulipita mpaka pale usingizi uliponipitia na kulala kabisa. Ila nilikuja kuamka majira ya kama saa nane ama tisa hivi za usiku, hiyo ni kutokana na makadirio yangu tu. Nilistuka sana pale nilipofungua macho. Nilikuwa katika sehemu ambayo sikuifahamu kabisa.
Je ni sehemu gani hiyo, usikose sehemu inayofuata.
Post a Comment